Kibali cha kutiririsha majitaka kwenye vyanzo vya maji ni miongoni wa vibali vinne vitolewavyo na Bodi ya Maji Bonde la Pangani. Kibali hiki hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009, Kifungu Na. 63 ambacho kinaeleza kuwa mtu yeyote mwenye uhitaji wa kutiririsha majitaka yatokanayo na shughuli za kiuchumi, viwanda, kilimo, au miundombinu anapaswa kuomba kibali cha kutiririsha majitaka hayo katika Bodi ya Maji Bonde la Pangani. Kibali hiki hudumu kwa muda wa mwaka mmoja hadi mitano kulingana mwenendo wa ubora wa majitaka yanayotibiwa baada ya kuzalishwa katika sehemu husika. Baada ya muda wa kibali kuisha, mteja anahitajika kuhuisha kibali pamoja na taarifa zake iwapo kuna mabadiliko yoyote ili kupata kibali kingine.
Hatua zifuatazo hufuatwa kabla ya kutolewa kwa kibali hiki lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa majitaka yanayozalishwa hutibiwa kufikia ubora wa viwango vilivyoweka na shirika la viwango Tanzania;
- Mwombaji kuandika barua ya ombi la kupata kibali na kuipitisha katika ofisi ya serikali ya kijiji, mtaa au kata kabla ya kuifikisha kwenye ofisi ya Bonde La Pangani
- Mwombaji kujaza fomu ya usajili
- Wataalamu kutembelea katika sehemu husika kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa awali juu ya shughuli zinazofanyika pamoja na kuchukua sampuli za majitaka ili Kufanya uchunguzi wa kimaabara.
- Bodi kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kama vile NEMC
- Ombi kupitishwa katika kikao cha Bodi
- Mwombaji Kupata kibali
Aidha, Hatua hizi huenda sambamba na malipo ya Gharama mbalimbali.
NB; Hatua Na. iv, v, vi huendelea endapo uchunguzi wa kimaabara utaibini kuwa viwango vya ubora wa majitaka baada ya kutibiwa vinakidhi viwango vilivyowekwa na shirika la Viwango Tanzania.